Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama Ndg. Timothy Ndanya amewataka Maafisa Watendaji Kata wa Mkoa wa Shinyanga Kulinda haki na misingi ya utawala bora kwa wananchi wanaowaongoza. Ameyasema hayo mapema leo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Watendaji Kata wa Mkoa wa Shinyanga kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama yaliyoratibiwa na tume ya haki za binadamu.
Bwana Ndanya amewaasa watendaji kufanya kazi kwa kuzingatia sheria zilizopo kwani kuna mambo mengi ambayo yanatokea lakini haki hazisimamiwi ipasavyo kitu ambacho kinasababisha malalamiko kwenye jamii.
"Mafunzo haya yawe chachu ya kuleta ari na mwamko wa mabadiliko miongoni mwetu katika kulinda, kutetea na kudumisha haki za binadamu nchini hasa katika mkoa wetu huu wa Shinyanga, kila mmoja wetu ahakikishe elimu hii inasambaa kuanzia ngazi ya familia hadi katika maeneo yetu ya kazi" Amesema Ndanya.
Awali akitoa neno la utangulizi Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mipango, Sera, ufuatiliaji na Tathmini ambaye pia ni Mratibu wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za binadamu Ndg. Laurent Burilo amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watendaji wa Kata wote nchini ili waweze kupata uelewa wa masuala ya haki za bibadamu na misingi ya utawala bora.
Mafunzo haya ni ya siku mbili kuanzia leo Tarehe 8/1/2019 hadi kesho tarehe 9/1/2019 na yamejumuisha Maafisa watendaji Kata wote wa Mkoa wa Shinyanga.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa