Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Balozi Seif Ali Iddi alisema kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Mkoani Shinyanga kwa ukusanyaji wa Mapato imeleta tija kubwa inayoshuhudiwa na Kila Mtanzania.
Alisema ujenzi wa Jengo kubwa la Hospitali linalotarajiwa kutoa huduma kwa Wananchi wa Mkoa Shinyanga pamoja na Wilaya jirani zinazouzunguuka Mkoa huo ni uthibitisho wa Kazi hiyo inayofanywa chini ya uelekezi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Watendaji wa Hospitali ya Mji Kahama, Viongozi wa Wilaya, Mkoa na Wananchi waliofika kupata huduma za Afya mara baada ya kulikagua Jengo kubwa la kuhudumia Wagonjwa linalojengwa kwa Fedha za ndani za Halmashauri ya Mji wa Kahama.
Alisema uthibitisho unaonyesha wazi kwamba Halmashauri ya Mji wa Kahama haina matapeli wala wababaishaji kutokana na muamko mkubwa iliyonayo kitendo ambacho ni alama inayotakiwa kwa Uongizi wowote unapopewa dhamana lazima uache alama itakayokuwa Historia ya uwepo wao.
Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga alifahamisha kwamba Ujenzi huo wa Jengo Jipya la Hospitali ya Kahama Mji lazima uende sambamba na matayarisho ya uwepo wa Watendaji watakaotosheleza kutoa huduma kwenye eneo hilo muhimu kwa ustawi wa Jamii.
Alieleza kwamba Taifa kuendelea kutegemea nguvu na misaada ya Mataifa ya nje ni hatari kutokana na wimbi la kulazimishwa kufuata mambo yaliyo kinyume na Mila na Utamaduni wa Asili uliozoeleka na unaopaswa kuendelezwa kwa faida ya Kizazi cha sasa na kile kijacho.
“ Kitendo hichi cha Wananchi wa Shinyanga kujitegemea wenyewe katika masuala yao ya Maendeleo na Uchumi kupitia Makusanyo ya Halmashauri zao kinanipa faraja mimi nikiwa Mlezi wa Mkoa na nastahiki kutembea kifua mbele mahali popote pale Nchini”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza na kumshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama kwa ubunifu na Uzalendo wake uliowezesha kuibua miradi mbali mbali ya Kiuchumi Wilayani Kahama ambayo imekuwa Mkombozi wa Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga.
Alisema uwepo wa eneo Maalum la Uwekezaji wa Viwanda Vikubwa na vile vidogo vidogo ni faraja kubwa hasa kwa kundi kubwa la Vijana waliopata fursa za kuendeleza miradi yao ya Ujasiri Amali inayokwenda sambamba na ujenzi wa Viwanda Vikubwa chini ya Wawekezaji Wazawa.
Akitoa Taarifa fupi ya Ujenzi wa Jengo hilo kubwa la Huduma za Afya katika Hospital hiyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mji wa Kahama Dr. Athumani Hussein Juma alisema ujenzi huo umezingatia ongezeko kubwa la Wagonjwa wanaohitaji huduma za Afya kwenye Hospitali hiyo.
Dr. Athumani alisema Jengo hilo loilianza ujenzi wake Mnamo Tarehe 2 Novemba Mwaka 2018 na lilitarajiwa kukamilika ndani ya Miezi 18 chini ya Ukandarasi wa Jeshi la Kujenga Taifa {Suma JKT} lakini changamoto zilizojitokeza ndani ya Mradi huo kwa sasa linatarajiwa kukabidhiwa Mwezi Juni Mwaka huu.
Alisema shilingi Bilioni 3.2 zitatumika katika ujenzi huo uliofikia asilimia 55% sasa na hadi kipindi hichi wajenzi wa mradi huo tayari wameshalipwa shilingi Bilioni 1.2.
Kaimu Mganga Mkuu huyo wa Hospitali na Mji wa Kahama alimueleza Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga kwamba Uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama uko mbioni kujenga Jengo Jipya kwa ajili ya huduma za Akina Mama Wajawazito na Watoto.
Alieleza kwamba lengo hilo uwepo wake litasaidia na kuchangia kudhibiti vifa vya akina Mama na Watoto wanaofikisha kwenye Hospitali hiyo inayotoa huduma za Wazazi kati ya 60 hadi 70 kwa Siku.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Zainab Rajab Telak alimshukuru Mlezi wa Mkoa huo Balozi Seif Ali Iddi na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi kubwa wanazochukuwa za ulezi wakizingatia zaidi huduma za Afya zinazohitajika kila siku.
Mh. Zainab alisema kitendo hicho mbali ya kuongeza baraka na upoendo lakini pia huleta faraja hasa kwa Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wanaokwenda kupata huduma za Afya wakisikia uwepo wa vifaa na zana zinazotolewa na Walezi hao Wawili.
Katika hafla hiyo Mke wa Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Mama Asha Suleiman Iddi alikabidhi Msaada wa Vifaa vya huduma za Wazazi ikiwemo Mipira ya Kuzalia, Gloves, Vigari vya Wagonjwa pamoja na zawadi kwa Wazazi waliojifdungua Usiku wa Kuamkia leo Tarehe 02 Machi 2020.
Mama Asha aliwaeleza Watendaji na Wagonjwa wa Hospitali hiyo kwamba ile ahadi yake ya kuwapatia Kifaa cha Uchunguzi wa Matumbo {Utra Sound} iko pale pale lakini kilichositisha ni hali ya mtihani uliopo Nchini Nchina ambako ndiko vinakonunuliwa vifaa hivyo.
Hata hivyo Mama Asha aliendelea kuwaasa Wauguzi wa Hospitali zote Nchini ikiwemo hiyo ya Mji Kahama kuendelea kuwa na lugha nzuri wakati wanapowahudumia Wazazi wanaofika kujifungua kwenye Hospitali na Vituo vya Afya.
“ Sote tunaelewa mazingira ya hatari anayokuwa nayo Mjazito ule wakati wa matayarisho ya kujiungua. Nusu Mfu na nusu hai kipindi kizito tunachopaswa kumpa faraja kubwa ili amalize salama mtiohani wake”. Alisema Mama Asha.
Alitanabahisha kwamba Mama Mjamzito anapokuwa katika Mtihani wa kutaka kujifungua anahitaji kupata Lugha nzuri kutoka kwa wale wanaomuhudumia ila apale faraja itakayomjengea nguvu kumaliza salama Mtihani huo.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa