"Tangazeni Mambo makubwa yanayotekelezwa na serikali" Waziri Mkuu
Imewekwa: March 18th, 2019
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini kuyatangaza na kuyatetea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano yanayoendelea nchini.
Pia, amewataka Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini kuhakikisha wanatumia vizuri taaluma zao na nyezo wanazopatiwa kueleza mambo yanayofanywa kwenye sekta zote na wasipofanya hivyo watatoa fursa kwa taarifa zinazosemwa na wapinga maendeleo kuonekana kuwa ni kweli.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini, kinachofanyika katika ukumbi wa BOT jijini Mwanza. Kikao hicho kinahudhuriwa na Maafisa Habari na Mawasiliano takbaribani 400.
Amesema maafisa hao wanatakiwa wakumbuke kuwa wanapaswa kuueleza umma wa Watanzania kwa kina masuala yanayofanywa na Serikali hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021) wenye kuweka msisitizo kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda.
“Mkumbuke kuwa kazi ya utoaji taarifa kwa wananchi kwa sasa si utashi binafsi wa mtoa habari bali hainabudi kufanywa kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi. Mathalan Sheria mpya ya Haki ya Kupata Taarifa Na. 12 ya mwaka 2016 yenye kuzitaka mamlaka za umma kuwapa wananchi taarifa zinazowahusu”.
Waziri Mkuu amesema sheria hiyo, inakwenda sambamba na sheria nyingine ya kumlinda mwananchi asilishwe taarifa za uongo, uchochezi na uzushi yaani Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016.