Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefungua kituo cha Kuwezesha Wananchi Kiuchumi Mjini Kahama. Kituo hiko ambacho kipo kwenye majengo yaliyokuwa yanatumiwa na Halmashauri ya Mji wa Kahama Kata ya Nyihogo kimefunguliwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Jenista Mhagama.
Akifungua kituo hiko Mhe. Mhagama amewaasa wananchi wa Kahama kuitumia fursa hii katika kujijenga kiuchumi kwani kituo kina mifuko yote muhimu kwa maendeleo ikiwemo kutoa Mikopo yenye riba nafuu na isiyo na riba, kutoa elimu ya ujasiriamali n.k. Mhe. waziri amewaahidi wananchi kuwa kituo kitatoa huduma muda wote na amewataka wataalamu wa vituo hivyo kutoa huduma kwa weledi.
Aidha Mhe. Waziri ameitaka Halmashauri kutenga fedha kwenye bajeti zake kwa ajili ya kukiendeleza kituo hiko.
"Niipongeze Halmashauri ya Mji wa Kahama kwa kutenga eneo la zaidi ya ekari 500 kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo, eneo lina viwanja zaidi ya mia sita vilivyopimwa na wafanyabiashara wamepewa bure kabisa, niombe na Halmashauri zingine kuiga huu mfano kwani tunahitaji kuona mfanyabiashara mdogo mdogo hanyanyasiki" Amesema Mhe. Mhagama.
Awali akitoa neno la Ukaribisho Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ndg. Albert Msovela ambaye ni Katibu tawala wa Mkoa wa Shinyanga amesema kuwa kituo hiko kimekuwa ni sehemu ya historia kwa Mkoa wa Shinyanga na ameahidi kuwa Mkoa kitakilea na kukitunza kituo hiko.
Ufunguzi wa kituo hiki ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim M. Majaliwa aliyoitoa Julai mwaka huu alipotembelea Wilayani Kahama na kujionea jitihada za kuwanyanyua vijana kiuchumi zinazofanya na Halmashauri ya Mji wa Kahama.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa