Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainabu Tellack ameongoza oparesheni ya kuwasaka Wafanyabiashara ambao sio waaminifu katika biashara zao. Oparesheni hiyo imefanyika Wilayani Kahama na hadi sasa zaidi ya Wafanyabiashara 11 wanashikiliwa na jeshi la Polisi kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za Kuuza Sukari za nje bila utaratibu, Kughushi mifuko ya makampuni ya ndani na kuweka sukari za makampuni ya nje, kupunguza ujazo wa bidhaa kwenye mifuko, kutofuata taratibu za uhifadhi wa bidhaa za Chakula katika Maghala n.k.
Akiongea katika zoezi hili Mhe. Tellack amesema kuwa lengo la Serikali ni kuona kuwa kila Mtanzania mfanyabiashara anafanya biashara kwa halali na kwamba wote waliokamatwa Sheria itafuata mkondo wake.
"hatuwezi kuruhusu kurudishana nyuma, wenye viwanda vya sukari wanasema sukari imejaa kwenye maghala yao haitoki kumbe kuna watu wachache wanahujumu jitihada za wenzao kwa 'kutotolesha' mifuko na kutumia kuweka sukari za nje, hili halikubaliki na nawahakikishia wote wanaohusika sheria itachukua mkondo wake" Alisema Telack.
Katika hatua nyingine Mhe. Telack amemuagiza mtaalamu wa TFDA Kahama kuhakikisha hakuna duka linaloweka nje bidhaa za chakula ambazo huwa zinapigwa jua na kupelekea kupoteza ubora na kuhatarisha afya za walaji.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa