Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli asubuhi ya leo amezindua kiwanda cha kuchakata vyuma eneo la Nyasubi Wilayani Kahama. Akiwa kwenye uzinduzi huo Rais ameahidi kusimamia sekta ya viwanda kwa hali na mali na amewaomba mawaziri na viongozi wa ngazi mbalimbali kuendelea kuvithamini viwanda vya ndani na kutumia bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi.
"Niwatake wakandarasi na viongozi wa Wizara, hususan Wizara ya Maji, na ninaposema wizara ya maji namaanisha taasisi zote zinazoshughulika na Maji zikiwemo Halmashauri wanapokuwa na Miradi ya Maji ni vyema wakatumia mabomba yaliyotengenezwa na wazawa, wakikosa ndio wafikirie kutafuta nje" Amesema Rais
Aidha Mhe. Rais amewaasa wamiliki wa viwanda wazawa kutengeneza bidhaa zenye ubora ili waweze kuaminika. Amesema kuwa kutengeneza bidhaa zilizo chini ya kiwango ndio sababu ya watu kuzikimbia bidhaa za ndani.
Awali akisoma taarifa ya Kiwanda hiko, Mkurugenzi wa Kahama Oil Mill & Companies Bw. Mhoja amebainisha changamoto kadhaa zinazoathiri uendeshaji mzuri wa Kiwanda hiko. Kuwepo kwa Kodi kubwa katika uingizaji wa bidhaa za viwanda ni changamoto mojawapo inayosababisha kushuka kwa uzalishaji.
Akilijibu suala kodi Mhe. Rais ameshauri mmiliki wa kiwanda kufikiria kuanzisha kiwanda cha uchimbaji chuma badala ya kuagiza chuma kilichokamilika kutoka nje ambacho katika misingi ya kodi inachajiwa kama bidhaa iliyokamilika badala ya Malighafi.
"wewe niambie unataka eneo lenye ukubwa gani ili uanzishe uchimbaji wa chuma, sheria za kodi zitaendelea kubana iwapo utaendelea kuagiza vyuma kutoka nje, mimi nitakupa hilo eneo bure" amesema Rais.
Mhe. Rais ameshahitimisha ziara yake Mjini Kahama na ameshaondoka kuelekea Singida na Dodoma.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa