Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Ndg. Anderson Msumba ametimiza ahadi yake aliyoitoa Juni 2018 ya kuwapa msaada wa pembejeo vijana wote wenye nia ya kujiajiri katika Kilimo. Ahadi hiyo ameitimiza leo baada ya vijana 28 kujitokeza na kupewa pembejeo zenye thamani ya Sh. Milioni 14.
Akikabidhi pembejeo hizo kwa Wakulima, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha amesema kuwa vijana wengi wanashindwa kutumia fursa hiyo waliyopewa na wamekuwa wazembe wa kujiajiri. Amebainisha kuwa vijana wanapenda kupoteza muda wao kwenye 'kubeti' badala ya kujishughulisha na Kilimo.
Mhe. Macha ameitaka Halmashauri kuwa ifikapo tarehe moja mwezi wa pili kama vijana hawajajitokeza basi fedha zilizokuwa zimetengwa katika bajeti ya 2018/2019 ya kuwawezesha vijana kwenye kilimo wapewe wazee wenye uwezo wa kufanya kazi badala yao.
Aidha Mkurugenzi wa Mji wa Kahama Ndg. Anderson Msumba amebainisha kuwa tatizo la Vijana kutojitokeza kuchukua ruzuku hiyo ni kwamba wengi wao wanataka wapewe pesa badala ya pembejeo.
Msumba amesema kuwa vijana ukiwapatia pesa huwa urejeshaji wake unakuwa mgumu na ndio maana Halmashauri ya Mji wa Kahama imeamua kutoa pembejeo za Kilimo ili mwenye nia ya kulima apewe.
Halmashauri ya Mji wa Kahama mwaka wa fedha 2018/2019 imetenga jumla ya shilingi milioni 53.4 kwa ajili ya kuwaptia ruzuku vijana wanaojishughulisha na Kilimo lakini hadi sasa Shilingi Milioni 14 pekee ndio zilizotolewa kwa vijana 28 waliojitokeza na kuonesha nia ya kujikita kwenye kilimo.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa