Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Azza Hilal Hamad (CCM) amekabidhi msaada wa Vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 36.5 kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati sita zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Ushetu,Msalala na Kahama Mji wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Mheshimiwa Azza amekabidhi vifaa tiba hivyo leo Jumanne Oktoba 16,2018 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama,Anamringi Macha wakati wa Kikao cha Baraza la UWT wilaya ya Kahama kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Kahama.
Vifaa tiba hivyo ni pamoja na shuka 100,mashine za kupima damu,wingi wa damu,sukari,joto,mapigo ya moyo na vifaa vya kusaidia kujifungua kwa akina mama ambavyo kupatikana kwake kumetokana na jitihada za mbunge huyo kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinapungua mkoani Shinyanga.
Awali akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa tiba hivyo,Mheshimiwa Azza Hilal alisema kupitia Kampeni yake ya ‘Afya Yangu Mtaji Wangu’ na kuwajali akina mama aliamua kutafuta wadau kwa ajili ya kusaidia kumaliza changamoto ya uhaba wa vifaa tiba katika vituo vya afya na zahanati.
Alivitaja vituo vya afya vitakavyonufaika na msaada huo kuwa ni Mwendakulima,Mbika na Lunguya na zanahati ambazo ni Ngogwe,Kisuke na Bulige.
Akipokea vifaa tiba,Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha alimshukuru mbunge huyo kwa msaada huo na kubainisha kuwa ameunga mkono kwa vitendo ilani ya CCM na juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika kuboresha sekta ya afya.
Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Elias Kwandikwa ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi aliahidi kumuunga mkono mheshimiwa Azza kwa kutoa msaada wa vifaa tiba katika vituo vitatu vya afya wilayani Kahama.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa