Wananchi wa kata ya mwendakulima halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga wameingiwa na hofu baada ya magodoro 30 kutelekezwa katika kituo cha afya Mwendakulima huku haijulikana aliyeyapeleka hapo.
Akizungumza leo kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, Diwani wa Kata ya mwendakulima Pius Emmanuel alisema magodoro hayo yana muda mrefu sasa tangu yapelekwe katika kituo hicho cha afya na kwamba taarifa zinadai kuwa gari ambayo haijajulikana ni ya kampuni gani ilifika eneo hilo na kuyashusha magodoro hayo na kuondoka pasipo kusema nani amewaagiza kuyapeleka.
Emmanuel ameiomba halmashauri kwenda kuyaondoa magodoro hayo na kuyafanyia vipimo kwani yanatishia amani kwa wananchi wa kata hiyo kutokana na kuhofu kuwa huenda yanasumu ama madhara kwa binadamu.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa kahama ABEL SHIJA amemwagiza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo ANDERSON MSUMBA kuhakikisha yanaondolewa kwenye kituo hicho cha afya na kupelekwa kituo cha Polisi kwa hatua za kupata RB na kufanya upelelezi kubaini nani aliyeyapeleka katika kituo hicho.
Akijibu kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mji wa Kahama, Kaimu Mganga mkuu wa halmashauri hiyo Dokta LUCAS DAVID amesema ofisi yake inataarifa na jambo hilo ambapo tayari wameanza mchakato wa kuyafuatilia ili kufahamu yamepelekwa na kampuni au na mtu gani katika kituo hicho cha Afya na kwamba wamekwisha litaarifu jeshi la Polisi wilayani Kahama kwaajili ya uchunguzi zaidi.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa